UFAFANUZI JUU YA USALAMA WA BIDHAA YA “CHAMA SNACKS”

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
TAARIFA KWA UMMA
27 Machi, 2017
UFAFANUZI JUU YA USALAMA WA BIDHAA YA “CHAMA SNACKS”

  1. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imebaini uwepo wa video clip inayosambazwa kupitia mtandao wa kijamii wa “WhatsApp” kuhusu bidhaa ya “Chama Snacks". Video hiyo inaonesha mtu akichanganya bidhaa ya Chama snacks na maji, kuikanda katika kiganja cha mikono na hatimaye kupata matokeo ya mchanganyiko wa kitu kinachovutika. Aidha, katika video hiyo inaelezwa kuwa matokeo hayo ni hatari kwa afya.

  2. Tunapenda kuutarifu umma kuwa maelezo ya video hiyo si ya kweli na yanapaswa kupuuzwa kwa kuzingatia uchunguzi na ukaguzi uliofanywa na TFDA.

  3. Kwa mantiki hiyo, wananchi wanaaswa kuacha kusambaza video hiyo potofu kwa kuwa maelezo yake hayana ukweli wowote na badala yake hujenga hofu miongoni mwa jamii.

  4. TFDA inatambua uwepo wa bidhaa ya Chama Snacks katika soko pamoja na bidhaa nyingine za jamii hiyo ambazo huzalishwa na viwanda vya ndani na nje ya nchi. Aina ya viambato vinavyotumika katika kuzalisha bidhaa hizo vimethibitishwa kukidhi vigezo vya usalama na ubora na uzalishaji wa bidhaa huzingatia mifumo bora ya uzalishaji.

  5. Kwa kuzingatia kwamba malighafi inayotumika katika uzalishaji wa bidhaa za aina hiyo ina wanga kwa wingi na teknolojia ya uzalishaji wake ambayo ni joto la juu la sentigredi 220 kwa muda mfupi (kwa lugha ya kitaalam hujulikana kama thermoplastic extrusion), ni dhahiri kuwa bidhaa hizo zinapochanganywa na maji na kukandwa huweza kutoa mchanganyiko wa kitu kinachonata na si kuvutika kama ilivyooneshwa kwenye video inayosambazwa.

  6. Kama ilivyo kwa bidhaa nyingine za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, bidhaa ya Chama Snacks na bidhaa nyingine za jamii hiyo zimesajiliwa na TFDA na hufuatiliwa katika soko kupitia mifumo iliyopo ya udhibiti ili kujiridhisha kuwa zinaendelea kukidhi vigezo vya usalama na ubora kwa lengo la kulinda afya ya mlaji.

  7. Wito unatolewa kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TFDA katika kutoa taarifa pindi wanapokuwa na mashaka juu ya usalama na ubora wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

  8. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kupitia ofisi za TFDA Makao Makuu zilizopo Mabibo External, Dar es Salaam, Ofisi za Kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mtwara na Tabora au kupitia barua pepe ya info@tfda.go.tz.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na Dawa
S.L.P. 77150
Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751/658 445222/777 700002 Nukushi: +255 22 2450793
Barua pepe: info@tfda.go.tz/ Tovuti: www.tfda.go.tz

English