UFAFANUZI KUHUSU UVUMI WA MADHARA YA DAWA ZA KUTIBU UGONJWA WA MALARIA

TAARIFA KWA UMMA
27 Machi, 2017
UFAFANUZI KUHUSU UVUMI WA MADHARA YA DAWA ZA KUTIBU UGONJWA WA MALARIA

  1. Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu dawa za kutibu malaria zenye kiambato kimoja (monotherapy) kuwa ni hatari, zinasababisha figo kutofanya kazi na pia kusababisha vifo. Dawa zilizohusishwa katika uvumi huo ni dawa aina ya vidonge na kapsuli zenye viambato vya Dihydroatemesinin, Amodiaquine, Artesunate, Artemether, Pyrimethamine, Halofantrine na Proguanil.

  1. Tunapenda kufafanua kwamba hadi kufikia mwaka 2014 dawa za kutibu malaria zilizotajwa na zenye kiambato kimoja (monotherapy) zilifutiwa usajili na kuzuiwa uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi nchini kutokana na tafiti kuonesha kuwa matumizi ya dawa hizo pekee husababisha usugu wa vimelea vya malaria. Aidha, dawa yenye mchanganyiko wa Halofantrine iliondolewa kwenye soko kwani ilibainika kusababisha madhara ya moyo.

  1. Hivi sasa dawa zilizosajiliwa na kutumika kwa ajili ya kutibu malaria ni zile zenye mchanganyiko wa viambato zaidi ya kimoja (mseto) kama vile dawa chaguo la kwanza katika kutibu malaria yenye viambato viwili vya Artemether na Lumefantrine. TFDA inasisitiza kwamba dawa husika hazisababishi figo kutofanya kazi au kifo endapo zitatumika kwa usahihi kama ilivyoshauriwa na Daktari.

  1. Dawa za kutibu malaria, kama ilivyo kwa dawa nyingine, zina madhara yanayofahamika ikiwa ni pamoja na kusababisha kuumwa kichwa, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, uchovu, maumivu ya misuli, kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika na kuwashwa mwili. Aidha, tahadhari inatakiwa kuchukuliwa endapo mgonjwa anayetumia dawa hizo atakuwa na matatizo ya moyo, mjamzito au ananyonyesha.

  1. Wananchi wanaombwa kuwasiliana na TFDA endapo watabaini au kuhisi kwamba dawa walizotumia zimesababisha madhara ya kiafya kwa kutoa taarifa kupitia mifumo ya utoaji taarifa za madhara ya dawa kwa njia ya kielektroniki www.tfda.go.tz/adr au kujaza fomu maalum zilizopo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kuziwasilisha TFDA Makao Makuu au katika ofisi zake za kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara na Tabora au kupitia ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya.

  1. Mwisho, wito unatolewa kwa wananchi kuepuka kusambaza taarifa zisizohakikiwa na TFDA kupitia mitandao ya kijamii ili kuondoa hofu na taharuki zisizo za lazima.

Imetolewa na;
Mkurugenzi Mkuu,

Mamlaka ya Chakula na Dawa,
S.L.P. 77150,
Dar es Salaam.
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751/658 445222/777 700 002
Nukushi: +255 22 2450793
Baruapepe: info@tfda.go.tz Tovuti: www.tfda.go.tz.

English