UFAFANUZI KUHUSU USALAMA WA MAFUTA YA ALIZETI

TAARIFA KWA UMMA 24 Aprili, 2017

UFAFANUZI KUHUSU USALAMA WA MAFUTA YA ALIZETI

  1. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imebaini uwepo wa taarifa iliyotolewa mnamo tarehe 23/4/2017 katika vyombo vya habari zinazotoa tahadhari juu ya usalama wa mafuta ya alizeti kutokana na mbegu za alizeti kuchafuliwa na sumukuvu ijulikanayo kama Aflatoxin.

  2. Tahadhari hiyo inatokana na matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2014/15 na wataaalam kutoka Michigan State University Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambao ulihusu mbegu za alizeti na mashudu kuchafuliwa na Aflatoxins.

  3. TFDA imefanya uchambuzi wa awali wa matokeo ya utafiti huo na kubaini kwamba ulihusu mbegu za alizeti na mashudu pekee na hivyo hautoshelezi kuthibitisha kuwa mafuta ya alizeti yamechafuliwa na Aflatoxins kwa kiwango ambacho ni hatarishi.

  4. Kwa mantiki hiyo, wananchi waendelee kuyatumia mafuta ya alizeti hasa yaliyothibitishwa na TFDA bila wasiwasi wowote.

  5. Pamoja na maelezo haya, tunapenda kuutaarifu umma kwamba, TFDA imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali kuhusiana na uchafuzi wa sumukuvu katika nafaka, karanga na bidhaa zake kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitafiti za ndani na nje ya nchi na kutoa tahadhari pale ilipobidi. Utafiti wa hivi karibuni umefanyika katika mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro na Manyara kati ya mwezi wa Juni 2016 hadi Januari 2017 na hatua stahiki zilichukuliwa.

  6. Hivyo, TFDA itafanya uchambuzi wa kina wa matokeo ya utafiti uliochapishwa katika jarida la PLOS One na kufanya ufuatiliaji na uchunguzi zaidi wa mbegu, mashudu na mafuta ya alizeti yanayozalishwa hapa nchini.

  7. Wito unatolewa kwa watafiti nchini wanaofanya tafiti kuhusu usalama na ubora wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi kuishirikisha TFDA kama mdau muhimu juu ya matokeo ya tafiti zao ili yatumike katika kuimarisha mifumo ya udhibiti na hivyo kulinda afya ya jamii.

  8. Rai inatolewa kwa vyombo vya habari kuwasiliana na TFDA ili kupata maoni na tafsiri sahihi kuhusu matokeo ya tafiti za kisayansi zinazohusu usalama na ubora wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi kabla ya kuzichapisha ili kuondoa uwezekano wa kuleta hofu kwa jamii.

  9. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kupitia ofisi za TFDA Makao Makuu na ofisi za Kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Mtwara na Tabora au kupitia barua pepe ya info@tfda.go.tz.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na Dawa

S.L.P 77150
Dar es Salaam
www.tfda.go.tz

Undefined