UFAFANUZI KUHUSU UVUMI WA DAWA AINA YA P-500® (PARACETAMOL) YA APEX LABORATORIES PRIVATE LIMITED-TAMIL NADU-INDIA

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU UVUMI WA DAWA AINA YA P-500® (PARACETAMOL)  YA APEX  LABORATORIES PRIVATE LIMITED-TAMIL NADU-INDIA

1. Mamlaka ya Chakula na Dawa  (TFDA) ni wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yenye jukumu la kudhibiti usalama, ubora na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

2. Kwa lengo la kujiridhisha kuwa dawa zilizopo nchini zinakidhi usalama, ubora na ufanisi, Mamlaka imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti ikiwa ni pamoja na mifumo ya tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara, ufuatiliaji wa usalama na ubora wa dawa kwenye soko.

3. Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu dawa aina ya P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na Apex  Laboratories Private Limited-Tamil Nadu-India kuwa ina virusi aina ya ‘Machupo’ vinavyosababisha ugonjwa wa “Bolivian Hemorrhagic Fever (BHF). Dawa hiyo ni kama inavyoonekana kwenye picha.

4. TFDA inapenda kuutaarifu umma kuwa dawa aina ya P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na kiwanda cha Apex  Laboratories Private Limited-Tamil Nadu-India haijasajiliwa na haipo kwenye soko la Tanzania.

5. Aidha, Mamlaka inawahakikishia wananchi kwamba kupitia mifumo iliyopo itaendelea kufuatilia kwenye soko na mipakani ili kuhakikisha kuwa pamoja na bidhaa nyingine, dawa hiyo ambayo haijasajiliwa haiingii nchini bila kufuata taratibu za usajili.

6. Wito unatolewa kwa wananchi kuwa endapo watabaini au kuhisi kwamba dawa walizotumia zimesababisha madhara ya kiafya wasisite kutoa taarifa TFDA kupitia mifumo ya utoaji taarifa za madhara ya dawa kwa njia ya kielektroniki www.tfda.go.tz/adr au kujaza fomu maalum na kuziwasilisha katika ofisi za Kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara na Tabora au kupitia ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya.

7. Mamlaka inawaomba wananchi kutoendelea kusambaza taarifa za uvumi ambazo zinalenga kuwaogofya na kuzua taharuki kwa wananchi kabla ya kupata ufafanuzi kutoka katika Mamlaka husika.

Imetolewa na;

Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa,
S.L.P 77150,
  Dar es Salaam.
Simu:    +255 22 2452108/2450512/2450751/658 445222/777 700 002
Nukushi: +255 22 2450793
Baruapepe: info@tfda.go.tz
Tovuti: www.tfda.go.tz

English