Ufafanuzi Kuhusu Taarifa Iliyotolewa Kupitia Gazeti La Mtanzania La Tarehe 25 Oktoba 2016 Yenye Kichwa Cha Habari “Tfda Mbeya Kikwazo Kwa Viwanda Vidogo”

  1. Mnamo tarehe 25 Oktoba, 2016 gazeti la Mtanzania lilitoa taarifa kuwa TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) ni kikwazo kwa maendeleo ya viwanda vidogo,  taarifa ambazo ziliandikwa na mwandishi Gordon Kalulunga.
  2.  TFDA inakanusha habari hizo kuwa siyo sahihi bali ni za upotoshaji.
  3.  Pamoja na jukumu ya kulinda afya ya jamii, TFDA inatambua kuwa inao wajibu wa kusaidia katika kuendeleza viwanda vidogo kwa sababu vina umuhimu katika kuongeza kipato cha wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Aidha, usalama wa bidhaa ni sharti muhimu katika biashara ya kitaifa na kimataifa, kwa hiyo kuwasaidia wasindikaji kuzalisha bidhaa salama ni kuwaongezea uwezo wa ushindani katika biashara.
  4. TFDA imekuwa ikitoa mafunzo kila mwaka ili kuwasaidia wasindikaji wadogo kukidhi masharti ya kisheria yanayolenga kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha ni salama kwa matumizi ya binadamu. Katika kipindi cha mwaka 2015/16 TFDA ilitoa mafunzo kwa wajasiriamali 224. Pia, TFDA imekuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi na wadau wengine ambao wanalenga katika kuwasaidia wajasiriamali.
  5. Ili bidhaa iweze kusajiliwa na TFDA, mzalishaji anapaswa kuzingatia masharti ya kisheria ambayo yanalenga kuhakikisha kuwa bidhaa inayozalishwa ni salama kwa matumizi ya binadamu. Vigezo vya kuzingatia ni pamoja na usajili wa majengo, hatua za uzalishaji, udhibiti wa ubora na wataalam wanaosimamia uzalishaji.
  6. Wasindikaji wadogo wanakumbushwa kuzingatia misingi bora ya uzalishaji bidhaa ili kumlinda mlaji na pia biashara zao ziweze kumudu ushindani wa kibiashara  kitaifa na kimataifa.  
  7. TFDA inatoa rai kwa waandishi wa habari kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kutoa taarifa ili wananchi waweze kunufaika zaidi na taarifa chanya katika  kuleta matokeo yatakayosaidia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwa umma.

 

Mkurugenzi Mkuu

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)

S. L. P 77150

Dar-es-Salaam, Tanzania

Simu: +255 22 658 445 222; +255 22 777 700 002

Barua pepe: info@tfda.go.tz

Tovuti: www.tfda.go.tz

English